Genesis 9

Mungu Aweka Agano Na Nuhu

1 aNdipo Mungu akambariki Nuhu na wanawe, akiwaambia, “Zaeni mkaongezeke kwa idadi na mkaijaze tena dunia. 2 bWanyama wote wa duniani, ndege wote wa angani, kila kiumbe kitambaacho juu ya ardhi, na samaki wote wa baharini wamekabidhiwa mikononi mwenu, nao watawaogopa na kuwahofu. 3 cKila kitu chenye uhai kiendacho kitakuwa chakula chenu. Kama vile nilivyowapa mimea mbalimbali, sasa nawapa kila kitu.

4 d“Lakini kamwe msile nyama ambayo bado ina damu ya uhai wake, kwa maana damu ni uhai. 5 eHakika damu ya uhai wenu nitaidai. Nitaidai kutoka kwa kila mnyama. Kutoka kwa kila mwanadamu pia nitaidai kwa ajili ya uhai wa mtu mwenzake.
6 f“Yeyote amwagaye damu ya mwanadamu,
damu yake itamwagwa na mwanadamu,
kwa kuwa katika mfano wa Mungu,
Mungu alimuumba mwanadamu.

7 gKuhusu ninyi, zaeni mwongezeke kwa wingi, mzidi katika dunia na kuijaza.”

8Ndipo Mungu akamwambia Nuhu na wanawe pamoja naye: 9 h“Sasa mimi ninaweka Agano langu nanyi, pamoja na uzao wenu baada yenu, 10pia na kila kiumbe hai kilichokuwa pamoja nanyi: Ndege, wanyama wa kufugwa na wanyama wote wa porini, wale wote waliotoka katika safina pamoja nanyi, kila kiumbe hai duniani. 11 iNinaweka Agano nanyi: Kamwe uhai hautafutwa tena kwa gharika, kamwe haitakuwepo tena gharika ya kuangamiza dunia.”

12 jMungu akasema, “Hii ni ishara ya Agano ninalofanya kati yangu na ninyi na kila kiumbe hai kilicho pamoja nanyi, Agano kwa vizazi vyote vijavyo: 13 kNimeweka upinde wangu wa mvua mawinguni, nao utakuwa ishara ya Agano nifanyalo kati yangu na dunia. 14Wakati wowote ninapotanda mawingu juu ya dunia na upinde wa mvua ukijitokeza mawinguni, 15 lnitakumbuka Agano langu kati yangu na ninyi na viumbe vyote vilivyo hai vya kila aina. Kamwe maji hayatakuwa tena gharika ya kuangamiza uhai wote. 16 mWakati wowote upinde wa mvua unapotokea mawinguni, nitauona na kukumbuka Agano la milele kati ya Mungu na viumbe vyote vilivyo hai vya kila aina duniani.”

17Hivyo Mungu akamwambia Nuhu, “Hii ndiyo ishara ya Agano ambalo nimelifanya kati yangu na viumbe vyote vilivyo hai duniani.”

Wana Wa Nuhu

18 nWana wa Nuhu waliotoka ndani ya safina ni: Shemu, Hamu na Yafethi. (Hamu ndiye alikuwa baba wa Kanaani.) 19 oHawa ndio waliokuwa wana watatu wa Nuhu, kutokana nao watu walienea katika dunia.

20Nuhu akawa mkulima, akawa mtu wa kwanza kupanda mizabibu. 21 pAlipokunywa huo mvinyo wake akalewa na akalala uchi kwenye hema lake. 22 qHamu, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake na kuwaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje. 23Lakini Shemu na Yafethi wakachukua nguo wakaitanda mabegani mwao wote wawili, kisha wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao. Nyuso zao zilielekea upande mwingine ili wasiuone uchi wa baba yao.

24Nuhu alipolevuka kutoka kwenye mvinyo wake na kujua lile ambalo mwanawe mdogo kuliko wote alilokuwa amemtendea, 25 rakasema, “Alaaniwe Kanaani!
Atakuwa mtumwa wa chini sana
kuliko watumwa wote kwa ndugu zake.”

26 sPia akasema, “Abarikiwe Bwana, Mungu wa Shemu!
Kanaani na awe mtumwa wa Shemu.

27 tMungu na apanue mipaka ya Yafethi;
Yafethi na aishi katika mahema ya Shemu,
na Kanaani na awe mtumwa wake.”

28Baada ya gharika Nuhu aliishi miaka 350. 29 uNuhu alikuwa na jumla ya miaka 950, ndipo akafa.
Copyright information for SwhKC